Wanajeshi watatu wa Ukraine wameuawa na wengine wanane wakajeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaotaka kujitenga, katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Matukio hayo yanavuruga zaidi makubaliano ya kuweka chini silaha yaliyopewa jina la "Siku ya Kimya" ambayo yalianza kutekelezwa Jumanne wiki hii. Msemaji wa jeshi Andriy Lysenko amesema majeshi ya serikali yalishambuliwa mara 22 na makombora ya waasi, ijapokuwa jeshi hilo bado linauheshimu mpango wa kusitisha vita. Machafuko hayo mapya ya mashariki mwa Ukraine, ambako wapiganaji wamejitenga na serikali ya mjini Kiev inayoyaunga mkono mataifa ya Magharibi na kujitangazia "Jamhuri za watu wa Luhask na Donetsk", yamevuruga zaidi uwezekano wa kuanzishwa tena mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza mgogoro huo uliodumu miezi minane.